Mada hii ina lengo la kukufanya uyaelewe mapenzi. Si kukimbilia kuacha pale kunapotokea tofauti za hapa na pale na mwenzi wako wa maisha. Uvumilivu unahitajika, amini kwamba utamu wote unaoyazunguka ‘malavidavi’ kuna ugumu mkubwa.
Ni sehemu ya tatu. Hapa tunazungumzia elimu zaidi inayoweza kukukomboa wewe kwa kuheshimu hisia za mwenzako na wakati huo huo ukawa unajali za kwako. Kwa pamoja ndiyo utaweza kufanikiwa kuwa na moyo tulivu katika nyakati zote.
Ukiheshimu hisia za mwenzi wako na ukawa unajali za kwako, itakusaidia kukufanya uwe na tumaini chanya wakati wote. Wakati wa matatizo, hasa kipindi ambacho hampo kwenye maelewano mazuri, utabaki na imani kwamba yote yatakwisha.
Penda kuamini kuwa “hili nalo litapita” kwamba wakati ambao mwenzi wako amenuna, hataki kuzungumza na wewe, unachopaswa kufanya ni kuheshimu hisia zake na uamini kwamba mwisho atatulia na uhusiano wenu utaendelea kwa maelewano makubwa.
Ukitaka kulazimisha awe mchangamfu kwako kipindi ambacho amenuna, ni sawa na kukaribisha matatizo zaidi. Ni vema kuelewana, watu wengi wanakosea katika uhusiano wao kwa sababu hawatumii busara ili kuwaelewa wenzi wao pindi wanapoonesha hali tofauti.
Busara iendelee kuchukua nafasi. Maneno “hili nalo litapita” yawe somo kwako. Kwamba leo umerudi nyumbani, umetaka chakula cha faragha, mwenzako amekwambia hajisikii vizuri. Hutakiwi kupandisha mizuka na kusababisha nyumbani pasilalike kwa siku hiyo.
Badala yake unapaswa kuvumilia. Jiulize mmefanya tendo mara ngapi katika uhusiano wenu, iweje siku hiyo akwambie hajisikii? Ukilazimisha ni sawa na kumfanyia mwenzako ubakaji. Si ajabu akikuona unakuwa mkali, atakubali kukupa kwa shingo upande lakini si kwa ridhaa yake.
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi kwa maana, nyakati nyingine utalazimika kuvumilia mambo ambayo pengine yanakuumiza. Mko wawili na kujenga tafsiri ya mwili mmoja. Pengine hata makundi yenu ya damu ni tofauti. Ilivyo maumbile yenu ni hasi na chanya ndiyo na damu zenu zilivyo.
Tofauti hiyo mnaielewa na kuikubali, iweje siku ukirudi nyumbani ukimkuta amenuna na hataki kuzungumza na wewe ushindwe kuelewa? Hapo ndipo uvumilivu wako unahitajika. Ni kipindi ambacho busara zako zinapaswa kufanya kazi kwa asilimia 100. Usilazimishe afanye upendavyo wakati mwili wake haupo tayari.
Unaingia faragha na mwenzi wako. Ameshindwa kukuridhisha kabisa. Ni hekima zako kutambua kwamba siku hazilingani. Mbona siku nyingine anakupa mambo mazuri mpaka unasema ‘poo’? Tatizo ni nini? Pengine nishati za mwili wake kwa siku hiyo hazipo sawasawa na hata yeye mwenyewe hajui.
Ukimkejeli kuwa hajiwezi ni sawa na kumchinjia baharini. Siku zinazokuja atashindwa kabisa. Si kwa sababu uwezo wake ni mdogo, la hasha! Maneno yako ya kejeli na dharau ndiyo yatakayoufanya moyo wake usinyae na kukuogopa ndani kwa ndani. Fikra zake zitashambuliwa na ugonjwa hatari.
Si ugonjwa unaosababishwa na kirusi, hapana. Ni gonjwa la maneno litakaloshambulia ubongo wake. Kila mara kabla ya kuingia mchezo atakuwa na maswali ya kujiuliza. “Sijui leo nitashindwa tena?” “Nikishindwa itakuwaje?” “Atanitukana tena?” “Hivi mimi ni mgonjwa?”
Mwisho wa maswali hayo atahitimisha kauli kwa kusema: “Inawezekana mimi ni mgonjwa kweli ndiyo maana nashindwa kazi.” Amini kuwa kauli hiyo ndiyo ugonjwa hatari ambao utashambulia hisia zake na kuusababisha mwili ushindwe kufanya kazi sawasawa.
Ukitaka kuendelea kufurahia mapenzi ni vizuri umpe moyo mwenzi wako pale inapoonekana ameshindwa kutekeleza kazi ya faragha inavyotakiwa. Kaa naye vizuri na umueleze kwa lugha laini kwamba baadaye au siku inayofuata mtafanya tena kikamilifu na hakutakuwa na kushindwa.
Ikibidi msifie, mwambie kuwa yupo kamili kwa sababu kila siku mnapoingia kazini huwa unatosheka. Mueleze kuwa siku hiyo anasumbuliwa na uchovu au hajisikii vizuri. Maneno hayo utayaona madogo lakini yatamjenga ipasavyo. Yatamrejeshea ari na afya, kwa hiyo siku nyingine hatakuogopa.
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi. Hii imesababisha watu wengi kushindwa kushirikiana vema na wenzi wao. Jambo dogo la kumuelewesha mwenzake linakuwa tatizo mpaka uhusiano unageuka shubiri. Wawili walioitana majina matamu na yenye kupendeza, wanageuka maadui.
Wanatangaziana sifa mbaya. “Yule muoneni hivyo hivyo kwa nje, hajiwezi kabisa kitandani.” Ni maneno ambayo si mageni. Yanasababishwa na watu kutotambua thamani ya mapenzi, ugumu uliopo ili iwe rahisi kwao kupata alama A kwenye uhusiano wao. Mapenzi ni magumu lakini ni rahisi sana.
Kanuni ni moja tu, kuwa mwelewa. Unaona mwenzi wako anashindwa kukufikisha unapopataka, wewe una jukumu la kumwelewesha. Mfahamishe maeneo ambayo anatakiwa ayafanyie kazi ili ufurahie tendo. Amini kuwa ukifanya hivyo, itakuwa rahisi kwako. Mapenzi ni matamu sana.
No comments:
Post a Comment