Msanii wa muziki wa kizazi kipya Bongo Flava, Khalid Mohamed aka 'TID' anarejea tena kwenye medani ya filamu na kutoka na filamu yake ya Prisoner inayozungumzia maisha yake ya gerezani.
Akizungumza hivi karibuni, TID anayemiliki bendi ya Top Band, alisema kuwa ameamua kuandaa filamu hiyo ili kuweka hadharani maisha wanayoishi wafungwa wawapo gerezani.
TID alifungwa kifungo cha mwaka mmoja mwaka jana kutokana na kosa la kumjeruhi mtu akiwa klabu, lakini aliweza kutoka jela kutokana na msamaha wa rais mwishoni mwa mwaka jana.
Mwanamuziki huyo ambaye amebadilika kitabia mara baada ya kutoka jela, alisema kuwa amejifunza mambo mengi alipokuwa gerezani na anahitaji kutoa elimu kwa wananchi.
"Kule gerezani nimekutana na mambo mengi yanayotisha na yanayokwenda kinyume na haki za binadamu. Nimeona kuna haja ya kuandaa filamu hii, ili wengine ambao hawajawahi kwenda jela waweze kujifunza," alisema mwanamuziki huyo.
TID ni miongoni mwa wasanii wa Tanzania waliotoa mchango mkubwa katika medani ya filamu, hasa kutokana na ushiriki wake katika filamu ya Girl Friend, ambayo ilitoa hamasa kubwa kwa watanzania kushiriki filamu.
No comments:
Post a Comment